Katika enzi ya kidijitali, tafsiri ya Kiswahili inachukua nafasi muhimu katika kuwezesha upatikanaji wa maarifa kupitia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA). Makala hii inajadili jinsi tafsiri ya Kiswahili inavyotumika kama daraja kati ya watumiaji na maarifa ya kidijitali, kwa kutumia Nadharia ya Ufikiaji wa Maarifa na Nadharia ya Mawasiliano katika Tafsiri. Kwa kutumia mbinu ya uchambuzi wa maudhui na mahojiano ya kina na wataalamu wa lugha, TEHAMA, na watumiaji wa majukwaa ya kidijitali, ilibainika kuwa tafsiri ya Kiswahili hairahisishi tu mawasiliano, bali pia huchochea usawa wa maarifa, ukuzaji wa lugha katika nyanja za kiteknolojia, na ujumuishaji wa jamii katika maendeleo ya kidijitali. Hata hivyo, changamoto kama ukosefu wa istilahi sanifu na ushirikiano mdogo kati ya wataalamu wa lugha na teknolojia huathiri ubora wa tafsiri. Makala inapendekeza uwekezaji katika tafsiri bora, maendeleo ya istilahi bunifu, na ushirikiano wa kitaaluma ili kuhakikisha Kiswahili kinapata nafasi endelevu na thabiti katika mazingira ya TEHAMA