Makala hii inachunguza maana za majina ya asili ya watoto katika jamii ya Waasu. Malengo mahususi yakiwa kwanza kubaini majina ya asili ya watoto, na pili kueleza maana zilizobebwa na majina hayo. Utafiti huu ni wa kitaamuli hivyo umetumia usanifu wa kifenomenolojia. Watoataarifa waliohusika katika kutoa data ni 18 ambao wamepatikana kwa mbinu ya usampulishaji tabakishi na usampulishaji tajwa. Data za makala hii zimekusanywa kwa kutumia mbinu ya usaili na majadiliano ya vikundi lengwa; kisha zikachanganuliwa kwa mbinu ya kusimba maudhui. Nadharia ya Uumbaji iliyoasisiwa na Sapir (1958) ndiyo iliyotumika katika makala hii. Matokeo yamebainisha majina ya asili ya watoto 145. Maana za majina haya zimegawanyika katika makundi yafuatayo: majina yenye maana zitokanazo na imani kwa Mwenyezi Mungu, mahali mtoto alipozaliwa, wanyama, misimu ya miaka na siku, majanga, vyakula na matukio ya furaha. Utafiti huu una mchango mkubwa katika kuhifadhi historia, na utamaduni uliojificha katika lugha ya Kichasu. Hata hivyo, tafiti zaidi kuhusu majina zifanyike katika jamii nyingine kwani jamii zinatofautiana katika asili, historia, shughuli za kijamii na utamaduni