Makala hii ni sehemu ndogo ya utafiti wetu wa uzamifu ambao ulijikita kwenye mada Uchanganuzi wa Ubabedume katika Nyimbo Asili za Jamii ya Abagusii. Katika makala hii tumetathimini namna mandhari huchangia utunzi wa nyimbo asili za jamii ya Abagusii kuwasilishaji ubabedume. Katika utafiti huu tuliongozwa na nadharia ya Uchanganuzi Makinifu wa Matini ambapo tulilenga kutathimini namna ubabedume katika jamii ya Abagusii hujitokeza katika mandhari mbalimbali kwa kuangazia jumbe katika nyimbo asili za jamii ya Abagusii. Tumeangazia baadhi ya mandhari katika kijamii na kufafanua ni kwa namna gani yalichangia utunzi wa nyimbo asili za jamii ya Abagusii. Maudhui tuliyoangazia ni pamoja na; mandhari ya tohara, ndoa, burudani, kazi, na mandhari ya mapambano. Utafiti huu ulijikita katika jimbo la Kisii na Nyamira maeneo yaliyotambuliwa kwa mujibu wa katika ya 2010. Data za utafiti huu zilitokana na kusikiliza nyimbo asili kutoka kwenye mtandao wa Youtube, kusikiliza nyimbo asili alivyozirekodi Obuchi katika CD yake ya 2019. Tulisisikiliza nyimbo asili za jamii ya Abagusii kisha tukazinakili na kuzitafsiri hadi lugha ya Kiswahili matini ambayo yalikuwa data yetu ya uchanganuzi. Data nyingine muhimu ambazo zilitufaa katika utafiti huu zilitokana na usomaji wa tafiti zilizofanywa awali kwa kuangazia mada hii. Utafiti huu ulirutubika pia kwa kusoma tasnifu za awali zilizotokana na mada hii, majarida mbalimbali kuhusu mada hii, vitabu mbalimbali na makala tofautitofauti ambayo yalihusiana na mada hii. Mahojiano na wazee wa jamii ya Abagusii, mahojiano na wataalamu wa fasihi za Kiafrika pamoja na mwelekeo kutoka kwa wahadhiri wangu yalitufaa katika kufanikisha utafiti huu. Data ya utafiti huu ilichanganuliwa kwa mujibu wa lengo la utafiti huu katika msingi wa mhimili wa nadharia yetu. Uwasilishaji wa matokeo ya utafiti huu ulikuwa kupitia njia ya kithamano kama njia faavu zaidi ya kushughulikia mahusiano pamoja na masuala ya kijamii