Makala hii imechunguza bembezi kama mbinu ya uhawilishaji wa maarifa ya Kiafrika, kwa kuangazia jamii ya Watumbatu. Utafiti huu unalenga kuelewa mchango wa bembezi katika kuhifadhi na kueneza maarifa, maadili na tamaduni za jamii. Uchunguzi ulifanyika katika eneo la Zanzibar, ndani ya jamii ya Watumbatu, kwa kipindi cha miezi sita. Mbinu za utafiti zilizotumika ni ethnografia, ambapo data ilikusanywa kwa mbinu ya usaili na majadiliano ya vikundi. Watoa taarifa wa utafiti walikuwa wazee wa jamii, waimbaji wa bembezi, wazazi na wahadhiri wa fasihi simulizi. Data iliyopatikana ilichambuliwa kwa njia ya uchambuzi wa maudhui ili kubaini dhima ya bembezi katika uhawilishaji wa maarifa. Matokeo ya utafiti yanaonesha kuwa bembezi zina nafasi kubwa katika kukuza lugha, kueneza maadili na kudumisha mshikamano wa kijamii. Nyimbo hizi hufundisha watoto kuhusu heshima, mshikamano wa kijamii, kazi, dini na falsafa ya maisha, kwa kutumia urudiaji wa maneno, methali, tamathali za semi na mifano ya maisha halisi. Aidha, utafiti ulibaini kuwa bembezi za Watumbatu zinafanana na zile za jamii nyingine za Kiafrika, lakini zinajitofautisha kwa athari ya tamaduni za Kiswahili na Uislamu. Hitimisho la utafiti huu linaonesha kuwa bembezi ni sehemu muhimu ya fasihi simulizi na zinachangia kwa kiasi kikubwa katika kuhifadhi utamaduni, elimu ya jamii na kujenga utambulisho wa Kiafrika. Kwa hivyo, inahitajika juhudi za makusudi katika kuzihifadhi na kuzitumia bembezi kama nyenzo rasmi za elimu na utamaduni