Kufanikisha mawasiliano ndiyo dhima muhimu ya lugha. Makala haya ni zao la uchunguzi wa matumizi ya Kiswahili kwenye miktadha ya uchuuzi jijini Kisumu na mjini wa Kakamega. Inajenga hoja kwamba wachuuzi na wateja wao huitumia hazina ya lugha zao kwa namna ya kipekee inayofanikisha mchakato mzima wa uendeshaji wa shughuli za kibiashara kwenye miktadha ya uuzaji na sokoni. Kwenye mchakato wa mawasiliano baina yao na wateja, wachuuzi wana welekeo wa kuteka kutoka kwa hazina ya lugha zao - Kiswahili, Kiingereza, Sheng, pamoja na lugha za kiasili. Hata hivyo, uteuzi wa lugha, launi au hata msimbo utumiwao kwenye shughuli mahsusi ya uchuuzi hutegemea upekee na haiba ya wahusika, huduma au bidhaa na nia ya mchuuzi kukidhi mahitaji ya kimawasiliano ili kufanikisha mauzo. Kwa mwongozo wa na nadharia ya Umitindo iliyoasisiwa na Leech (1969) na kuendelezwa na Leech & Short (2007), uchunguzi huu wa kitaamuli ulijikita katika muundo mseto wa kitakwimu na wa kithamano. Kijiografia, eneo la utafiti huu ni jiji la Kisumu na mji wa Kakamega. Ulijishughulisha na uwanda wa sajili ya biashara ya uchuuzi kwenye taaluma ya Isimujamii. Kwa hivyo, Idadi lengwa ni wachuuzi 11,000 katika jiji la Kisumu na mji wa Kakamega. Jiji la Kisumu na mji wa Kakamega uliteuliwa kwa usampulishaji lengwa. Sampuli ya utafiti ilijumuisha wachuuzi 272, yaani 147 jijini Kisumu na 125 mjini Kakamega. Hata hivyo, usampulishaji nujumu ulitumika kuwashirikisha wachuuzi katika shughuli mbalimbali za uchunguzi. Data ya utafiti ilikusanywa kwa njia za uchunzaji na usaili wa ana kwa ana uliowashirikisha wachuuzi na wateja wao kwenye miktadha halisi ya biashara. Vifaa vilivyotumiwa kukusanyia data vilijumuisha mwongozo wa uchunzaji, mwongozo wa usaili, kinasa sauti na simu ya kisasa. Baada ya unukuzi, data ilichujwa, ikaainishwa na kusimbwa. Data ilichanganuliwa kwa mkabala mseto wa kitakwimu na kithamano na kuwasilishwa kwa njia ya majedwali, grafu, asilimia na kufafanuliwa kimaelezo kwa mwongozo wa malengo na mihimili ya nadharia ya Umtindo. Matokeo ya utafiti yamebaini kuwa Kiswahili ndiyo lugha biashara katika uendeshaji wa uchuuzi jijini Kisumu na mjini Kakamega. Utafiti huu utawachochea watafiti wengine kuchunguza sifa za matumizi ya lugha katika aina nyingine za biashara kando na uchuuzi..