Miaka ya hivi karibuni majina ya asili katika jamii nyingi za kitanzania yamekuwa yakikabiliwa na changamoto ya kupotea kwa kasi hasa kwa vijana kutokana na ujio wa sayansi na teknolojia pamoja na dini. Makala haya yamekusanya na kubainisha majina ya asili ya watu katika jamii-lugha ya Wagogo. Makala yameongozwa na swali moja katika kuandaliwa kwake. Swali hilo linauliza; Majina yapi ya asili ya watu yanayotumika katika jamii-lugha ya Wagogo? Mbali na kujadili swali hilo muhimu, Makala haya pia yametoa mapendekezo kuhusu njia za kuendeleza matumizi ya majina ya asili ya watu katika jamii-lugha husika. Data za makala zimekusanywa kwa mbinu ya mahojiano na majadiliano ya kundi lengwa na kuwasilishwa kwa njia ya maelezo na majedwali kwa ufafanuzi zaidi. Uchanganuzi wa data umeongozwa na Nadharia ya Uumbaji ya (Sapir-Whorf, 1958) inayosisitiza kwamba, lugha ndio msingi wa kuuelewa ulimwengu. Unapojifunza lugha hiyo hata dunia unayoiumba akilini mwako itatokana na dunia iliyoratibiwa na wasemaji wake. Matokeo ya uchunguzi wa makala haya yamedhihiridha kuwa, majina ya asili ya watu katika jamii-lugha ya Wagogo yapo katika makundi kulingana na jinsi yanavyotolewa au kupatikana. Makundi yamebainishwa kwa kuzingatia sifa zinazofanana katika makundi mbalimbali