Usohalisia ni kipengele muhimu kinachodhihirika katika tungo za kisasa za fasihi. Watunzi wa fasihi ya kisasa hutumia mtindo wa usohalisia kwa namna mbili kuu ambazo ni ujirejelezi wa mtunzi na usohalisia wa kihistografia. Makala haya yamefafanua jinsi usohalisia wa kihistografia ulivyotumika katika nyimbo teule za kisasa za injili za Kikamba. Nyimbo za kisasa za injili za Kikamba zimerejelewa ili kuwakilisha nyimbo za kisasa za injili zilizoimbwa kwa lugha yoyote nchini Kenya. Utanzu wa nyimbo za injili umeteuliwa kwa sababu kutoka miaka ya elfu mbili umedhihirisha mabadiliko si haba ya kuuwasilisha kwa hadhira bali na kuwa utanzu pendwa. Makala haya yametumia mtazamo wa kiusasaleo kuchanganua matini za nyimbo teule za kisasa za injili za Kikamba. Mtazamo wa kiusasaleo hushuku na kupinga mitazamo ya kijadi na kupendekeza mitindo mipya ya kuwasilisha tungo za fasihi ya kisasa. Kutokana na uchanganuzi, iligunduliwa kuwa matumizi ya mtindo wa usohalisia wa kihistografia yalidhihirika kwa namna kadhaa katika nyimbo za injili za kisasa za Kikamba zilizoteuliwa kuchunguzwa. Matumizi ya mtindo wa usohalisia yalidhihirika kupitia utumiaji wa mbinu mbalimbali ambazo zimefafanuliwa na makala haya