Logo Lanfrica

Mtazamo Mpya Kuhusu Lugha ya Kiswahili na Elimu ya Juu Nchini Tanzania

Domaine:

educationnatural language processing
Créateur:
MkwGer
Éditeur:
Dar
Hôte:
Makala haya yanahusu nafasi ya lugha ya Kiswahili katika mfumo wa elimu ya juu nchini. Msingi wake unatokana na ujumuishaji mno wa kimapokeo kwamba kila kinachofundishwa kwa ‘Kiswahili’ ni lugha ya Kiswahili. Uchambuzi wa sera na maandiko mengine yanayohusiana ama na lugha na elimu au lugha na utamaduni ulifanyika na kuwasilishwa kinathari. Vilevile, maudhui ya kozi za taaluma za Kiswahili zinazofundishwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (CKD) hususani katika Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI) yalifanyika. Matokeo ya uchambuzi huo yamedhihirisha kwamba lugha ya Kiswahili imevuka mipaka ya kufundishwa kama somo na kuwa lugha ya kufundishia taaluma za Kiswahili katika ngazi za shahada ya awali, umahiri na uzamivu. Hii ina maana kuwa lugha ya Kiswahili inatumika katika uzalishaji wa maarifa yanayotokana na tafiti. Tafiti ni sehemu ya masharti ya kukamilisha shahada za umahiri na uzamivu katika vyuo vikuu duniani. Licha ya ombwe la sera ya lugha ambalo ni kikwazo kikubwa cha upanuzi wa matumizi ya Kiswahili katika elimu ya juu nchini, mtazamo wa makala haya ni kwamba Kiswahili kinatumika kufundishia. Wito wa makala haya ni kwamba wigo wa matumizi ya Kiswahili kufundishia elimu ya juu upanuliwe katika nyuga zingine za kitaaluma baada ya kuonesha ufanisi katika taaluma za Kiswahili. Wito huu unatolewa kutokana na urazini thabiti kwamba Kiswahili bado hakitumiki kufundishia elimu ya sekondari. Maoni ya makala haya ni kwamba kutokutumika kwa Kiswahili katika ngazi hiyo, ni tatizo la wafanya maamuzi kuhusu lugha na elimu. Hatua madhubuti inayopaswa kuchukuliwa kwa mahali pa kwanza ni kuipa lugha ya Kiswahili hadhi ya kuwa lugha ya kufundishia elimu ya juu na elimu ya sekondari. Hatua ya pili ni kuhakikisha kwamba katiba ya nchi inaitambua lugha ya Kiswahili kuwa ni lugha ya Taifa. Hii itasaidia kuhalalisha upangaji wa rasilimali za kuendeleza lugha hiyo na kuchochea wigo mpana wa kufundishia kwa maslahi ya taifa.

Similaires