Katika kazi ya fasihi, mawazo, mafunzo na falsafa ya msanii hubainisha msimamo wake kuhusu masuala mbalimbali ya kijamii. Msimamo ni ile hali ya mwandishi kuamua kufuata na kushikilia jambo fulani. Jambo hili huweza kukataliwa na wengi lakini akalishikilia tu. Msimamo ndio huweza kuwatofautisha wasanii wawili au zaidi wanaoandika kuhusu mazingira yanayofanana. Hili ambalo msanii anashikilia sana ndilo tunaloita katika utafiti huu kuwa mwonoulimwengu wa mwandishi. Ni vyema kujiuliza ni mambo gani yanayomsukuma na kuchochea mwandishi Ken Walibora kuchukua mawazo, msimamo na mkondo fulani katika uandishi wake. Uchanganuzi huu ulinuia kuchunguza mwonoulimwengu wa Ken Walibora kwa kujaribu kudokoa mawazo na falsafa zake kama zinavyojitokeza katika kazi zake za kisanaa. Huu ulikuwa utafiti wa maktabani ulioongozwa na nadharia za uhalisia na mwingilianomatini kuchunguza mwonoulimwengu wa Ken Walibora kupitia yale anayosema kujihusu na yale wengine wanasema kumhusu kisha kuyalinganisha na kazi za fasihi alizoandika kwa lengo la kuona mfanano wa mwonoulimwengu wake kwa sababu mwonoulimwengu unaonekana kutokana na maudhui yanayoendelezwa katika kazi za kisanaa. Kwa kutumia mbinu ya uteuzi sampuli maksudi tuliteua vitabu sita: Siku Njema (1996), Damu Nyeusi (2008), Kidagaa Kimemwozea (2012), Nasikia Sauti ya Mama (2014), Mbaya Wetu (2014) na Kisasi Hapana (2008). Tulivilinganisha ili kutambua mfanano wa mwonoulimwengu wa Ken Walibora katika vitabu hivi. Tulitathmini mwonoulimwengu huu kwa kujaribu kuelewa namna anavyosuka maudhui katika kazi zake kwa sababu mwonoulimwengu hudhihirika katika maudhui. Utafiti huu utachangia katika kufanyiza akili, kupanua uelewaji, kunoa nguvu za kufikiri, kupanua mwono, kukuza uwazaji na hisi ya ujumui ambalo ni lengo kuu la kazi yoyote ile ya fasihi. Wasomaji wa kazi za Ken Walibora watapata kuelewa kazi zake vizuri zaidi kwa kuwa na picha kubwa ya msanii huyu akilini. Pia inaweza kuwa kichocheo kwa wasanii wapya ili kujua namna ya kupata maoni ya kusuka kazi zao