Matumizi ya ucheshi zimbwe katika mitandao ya kijamii kama vile X (Twitter), Tiktok, Facebook, Instagram na WhatsApp yameongezeka hasa miongoni mwa vijana katika ya Kenya. Haya yameshuhudiwa kwa ajili ya ukuaji wa teknolojia ya habari na mawasiliano kama vile simutamba, tarakilishi na intaneti. Utafiti huu ulikusudia kuchunguza namna wananchi wa Kenya hutumia ucheshi zimbwe kama njia ya kukabiliana na hali ngumu ya maisha ambayo huwakabili. Ugumu huu umekuwa ukisababishwa mifumuko ya bei za bidhaa ya mara kwa mara, ukosefu wa kazi, kutozwa kodi ya juu na serikali, ongezeko la vifo visababishwavyo na polisi, kuwepo kwa magonjwa mbalimbali na misukosuko ya kisiasa ambayo imekuwa ikishuhudiwa kuanzia mwaka wa 2017 hadi 2025. Haya yote yanayumkinika kusababishwa na mifumo ya uongozi na utawala usiowajali wananchi. Utafiti huu ulikuwa na malengo mawili: kuchunguza mbinu za kimtindo zinazotumika kujenga ucheshi zimbwe kwenye mitandao ya kijamii kama njia ya kukabiliana na hali ngumu ya maisha, pili ni kuhakiki mikakati ya kipragmatiki inayotumika kwenye mitandao ya kijamii katika kujenga ucheshi zimbwe. Utafiti huu uliongozwa na mihimili ya nadharia ya Ushiriki ya Grice (1975) ambayo inasema kuwa katika mazungumzo ya kila siku, msemaji na msikilizaji hufuata bila kujua kanuni za kushiriki. Utafiti huu ulifanyika kwenye mitandao ya kijamii kwa kupakua jumbe zilizokuwa na ucheshi zimbwe kisha kuzichanganua. Usampulishaji ulifanywa kwa njia ya kimakusudi mintarafu ya madhumuni ya utafiti. Utafiti huu ni wa kithamano na ulihusisha mbinu za kimaelezo katika uwasilishaji na uchanganuzi. Matokeo yalionyesha jinsi hali ngumu ya wananchi husababisha kufadhaika, msongo wa mawazo na kutamauka hubadilishwa na kuwa ucheshi. Ucheshi huu ni njia mwafaka ya kuondoa masumbuko na misongo ya mawazo, kukashifu viongozi kwa njia isiyo ya moja kwa moja na kushiriki ujitambulishaji miongoni mwa wanaoteseka. Ilidhihirika kuwa chuku, kejeli, kinaya na taswira hujenga jumbe zenye ucheshi zimbwe zinazotumika mno katika mitandao ya kijamii nchini Kenya. Ni wazi kwamba ucheshi zimbwe hautumiki tu kama njia ya kuchekesha bali hutumika kama mikakati ya kukabiliana na changamoto zinazomkaba na kumtatiza mwanadamu. Utafiti huu unaonyesha namna lugha, ucheshi zimbwe na matatizo ya kijamii kama vile ya kiuchumi huingiliana na maisha ya kisasa ya kidijitali ya Wakenya. Utafiti huu una mchango mkuu katika Isimu hasa Pragmatiki kwa kuonyesha namna ambavyo lugha hutumika katika mawasiliano ya mitandaoni kwa kuonyesha jinsi maana inavyojengwa hasa katika diskosi za mitandaoni.