
Makala haya yanahusu ujitokezaji wa ukiushi wa kisintaksia katika tamthiliya ya Kaptula la Marx. Katika makala haya mkabala wa kimaelezo na usampulishaji lengwa ulitumika. Data zilikusanywa kutoka maktabani kwa kutumia mbinu ya uchanganuzi matini na kuchambuliwa kwa kutumia mbinu ya kusimbisha maudhui. Mjadala wa matokeo ya utafiti umeongozwa na nadharia ya Umitindo iliyoasisiwa na Shykrovisky (1965). Baadae nadharia hii ikaendelezwa na wataalamu wengine kama vile; Leech na Short (2007), Agu (2008) na Wamitila (2008). Makala haya yanaonesha kuna ukiushi wa kisintaksia ambao umekiukwa na mwandishi katika tamthiliya teule. Lengo la kukiuka ni kujenga mtiririko mzuri wa mazungumzo baina ya wahusika katika kujenga visa na matukio ili kuibua maudhui. Kwa hiyo watafiti na wataalamu wa fasihi wanapaswa kujikita katika tanzu zote za fasihi andishi hasa kwenye tamthiliya ili kuchunguza ukiushi wa darajia ya ushikamani kisarufi na ukiushi wa darajia ya kileksika. Hii ni kutokana na ukweli kwamba ukiushi ndiyo moyo wa ubunifu wenye kudumisha uhai katika tanzu za fasihi.