Katika mchakato wa kufanya tafsiri ya matini kutoka lugha chanzi kwenda lugha lengwa, mara nyingi majina maalumu hayatafsiriwi. Makala haya ya uchokozi yanajaribu kufafanua kuwa majina mengi ya Wabantu, ya mahali, na ya vitu mbalimbali yana maana maalumu kama vile kuonesha tabia au hali ya mtu, kuonesha tabia au hali ya watu wa ukoo fulani au watu wa mahali fulani. Pia, majina mengi maalumu ya mahali yanatumika kuonesha tabia na matumizi ya eneo fulani kama vile sehemu ya mito, misitu, mapango, milima au vilele vya milima. Mbinu mahuluti zilitumika kupata data katika makala haya. Kwanza, ni mbinu ya maktabani; na pili, ni mbinu ya uwandani. Kwa kuzingatia mwega wa kisemantiki na kiisimujamii, data ziliwasilishwa na kuchambuliwa ili kuibua maana zinazoambatana na majina hayo. Makala haya yanahoji kuwa kuna maarifa mengi muhimu yanayoweza kupatikana kwa kutafsiriwa majina maalumu ya Kibantu. Tafsiri ya majina maalumu ya Kibantu inaweza kuelimisha jamii kuhusu historia ya mahali na watu wake, shughuli na mahusiano ya kijamii, ya kiuchumi, ya kisiasa, ya kiutamaduni, ya kiimani, na ya kisayansi na teknolojia. Makala yanahitimisha kwamba kama tunataka kupata maarifa jumuishi juu ya yale yaliyomo katika matini chanzi, hasa kuhusiana na maana ya majina maalumu, hatuna budi kutafsiri majina hayo kwa wingi kadiri inavyowezekana.