Utafiti huu unalenga kuchunguza athari zinazotokana na mtagusano wa lugha ya Kiswahili na Kikuyu kwa lugha ya Kishona. Shona ni kabila mojawapo la Wabantu ambao asili yao ni nchini Zimbabwe na walifika nchini Kenya zaidi ya miaka sitini iliyopita kama wamishenari. Kufikia sasa, Washona wametagusana na jamiilugha mbalimbali nchini Kenya katika Kaunti ya Kiambu inayojulikana kwa wingilugha hasa kwenye mitaa ya Kinoo, Kikuyu, Kiambaa, Gitaru, na Githurai. Mtagusano wa lugha unapotokea, lugha husika huathirika kwa viwango mbalimbali kama vile kwenye fonetiki, kifonolojia, kimofolojia, kisintaksia na hata kisemantiki. Utafiti huu uliongozwa na nadharia ya uthabiti wa kiisimujamii wa lugha iliyoasisiwa na Giles, Bourhis na Taylor (1977) na kuendelezwa na Landweer (2000) na nadharia ya uzalishaji kijamii ya Bourdieu (1977). Mawanda mawili yalihusishwa ambayo ni utafiti wa maktabani na wa nyanjani. Utafiti wa nyanjani ulifanyika katika makazi ya wanajamiilugha ya Kishona ili kupata data ya moja kwa moja iliyojibu swali la utafiti. Jumuiya ya utafiti ilikuwa kabila la Washona wanaoishi katika mitaa mitano ya kaunti ya Kiambu.Sampuli ya utafiti huu iliteuliwa kimaksudi na kwa njia elekezi. Mbinu zilizotumiwa katika ukusanyaji data ni pamoja na hojaji, mahojiano, uchunzaji, mijadala ya vikundi vidogovidogo na maswali mepesi yaliyoandaliwa kimbele. Data iliyokusanywa ilichanganuliwa kwa kutumia mbinu changamano. Matokeo yaliwasilishwa kwa njia ya maelezo, takwimu na asilimia huku yakiongozwa na nadharia mbili za utafiti. Kufuatia juhudi za UNESCO za kudumisha lugha asilia, utafiti huu ulikuwa wa manufaa kwa taifa la Kenya na mataifa mengine kwa kuwa uliongezea data muhimu katika kuhifadhi utamaduni wa Washona na mwelekeo wa udumishaji kwa lugha za kabila mbalimbali