Tangu jadi, binadamu amekuwa akitumia methali kutekeleza dhima muhimu katika jamii. Kwa hivyo, wanajamii wamekuwa wakitafuta njia za kutambulisha kila mshikadau katika shughuli za maendeleo ya kijamii kwa mujibu wa utamaduni wa jamii husika. Utafiti huu unahusu nafasi ya methali za Kiswahili katika kutambulisha watoto. Methali ni mojawapo wa vipera muhimu vya utanzu wa semi katika fasihi simulizi. Methali ni hazina adimu katika maisha yakila siku ya wanajamii maanake husheheni dhima mbalimbali katika jamii inayohusika. Mojawapo ya dhima hizo ni kuangazia hali zinazowazunguka wanajamii kama vile kutambulisha watoto ili kuweka wazi nafasi yao katika jamii. Kichocheo cha utafiti huu ni kwamba, mbali na kuwa methali za Kiswahili kuainishwa kwa mujibu wa miktadha na dhima zake, bado kuna pengo la maarifa katika uchunguzi wa utambulisho wa watoto ili kuwasilisha ujumbe wa methali husika. Utafiti huu umejikita katika malengo matatu mahususi ambayo ni kuchambua vipengele vinavyotambulisha watoto katika methali za Kiswahili, kudadavua mabadiliko ya mfumo wa kijamii katika utambulisho wa Watoto katika methali za Kiswahili na kutathmini athari za methali za Kiswahili katika kutambulisha watoto katika jamii. Tumetumia nadharia ya Semiotiki iliyoasisiwa na Ferdnand De Saussure na Charles Pierce. Data ya utafiti imekusanywa kutoka kwenye kamusi za methali kama vile - Kamusi ya Methali: Maana na Matumizi na Maelezo ya Methali za Kiswahili. Kamusi hizi zimeteuliwa kwa sababu zinaafikiana na malengo na nadharia ya utafiti. Usampulishaji lengwa ndio umetumiwa kuteua kamusi pamoja na methali zinazohusu utambulsho wa watoto katika kamusi teule. Tumechunguza methali 4,500 kwenye kamusi teule. Baadaye, tukateua methali 90 ambazo zinaakisi malengo ya utafiti wetu. Data imekusanywa maktabani kwa kusoma vitabu, makala na tasnifu mbalimbali kuhusiana na mada ya utafiti huu. Baada ya kukusanya data, imechanganuliwa kwa njia ya maelezo. Matokeo ya utafiti huu yatatumiwa na waandishi wa kazi hii ya fasihi kuelewa namna ya kuutambua ujumbe wa ndani kwenye methali ili kuzitumia ifaavyo. Vilevile, utatumiwa na watafiti wa baadaye katika kuendeleza tafiti kuhusu kipera hiki cha methali.