Utafiti huu ulichunguza na kuchanganua sababu za ubadilishaji msimbo katika mawasiliano baina ya wafanyabiashara na wanunuzi katika soko la Daraja Mbili. Soko hili ni maarufu miongoni mwa masoko yanayopatikana katika mji wa Kisii nchini Kenya. Ingawa wenyeji wa Kisii ni wa kutoka jamii ya Abagusii, soko hili huwaleta pamoja wauzaji na wanunuzi kutoka jamii mbalimbali nchini Kenya. Kwa kuzingatia kuwa Kenya ni nchi ya wingi-lugha, ubadilishaji msimbo hutokea mara kwa mara katika semi za wafanyabiashara na wanunuzi. Ili kubaini sababu maalum za ubadilishaji msimbo katika muktadha halisi wa soko hili, utafiti huu ulitumia data ya nyanjani iliyopatikana kwa njia ya uchunzaji, usaili na mahojiano baina ya mtafiti, wafanyabiashara na wanunuzi. Data ilikusanywa mwaka wa 2013 kuanzia mwezi wa Januari hadi Machi. Kisha, data ilichanganuliwa na kuwasilishwa kwa njia ya maelezo. Kwa ujumla, utafiti ulibaini kwamba wafanyabiashara na wateja wao hubadilisha msimbo baina ya Kiswahili, Kiingereza, na lugha za kijamii kama vile Ekegusii na Kijaluo. Kuna sababu kadha zinazochochea ubadilishaji msimbo, ambazo ni: ukosefu wa udhibiti wa msamiati wa kutosha na faafu wa Kiswahili kurejelea baadhi ya mambo katika uhalisia wa sokoni, nia ya kujenga mahusiano na ukaribu wa kibiashara, kujenga maafikiano, kurahisisha mawasiliano, kuimarisha umoja wa kimakundi, kudumisha usiri na wepesi wa kujieleza. Aidha, ubadilishaji msimbo hutumiwa kama mkakati wa kusisitiza mambo, na kujitambulisha kwa washirika katika mazungumzo. Hitimisho ni kwamba, ubadilishaji msimbo katika soko la Daraja Mbili hauwezi kuangaliwa kama tukio nasibu, tukio la sadfa au tukio lisilo na mpango, bali ni tukio la kimkakati na kimpango katika miktadha anuwai ya mawasiliano.