Utafiti huu ulichunguza mbinu za lugha katika nyimbo za mapenzi kwenye kipindi cha Mambo mseto cha Redio Citizen. Nadharia iliyotumika ni Nadharia ya mtindo iliyoasisiwa na Buffon (1930) na kuendelezwa na watafiti wengine. Muundo uliotumika ni mkabala mseto kuegemea muundo wa QUAL-quan. Sampuli za maksudi zilitumika kukiteua kipindi cha Mambo mseto na wanafunzi wa chuo kikuu cha kikatoliki cha Afrika Mashariki. Wanafunzi 83 kutoka chuo kikuu cha Kikatoliki cha Afrika mashariki walifanyiwa utafiti. Nyimbo saba kuashiria asilimia 30 kutoka jumla ya nyimbo ishirini na nne za mapenzi zilizochezwa ziliteuliwa. Uteuzi wa nyimbo hizo saba uliongozwa na maoni ya Fink (2003) anayesema kuwa, kwa watafitiwa chini ya 1000, jumla ya asilimia 30 ya usampulishaji hutumika. Hivyo katika utafiti huu, mtafiti alichukua ailimia 30 ya nyimbo 24 alizosikiza akapata nyimbo saba. Matokeo ya utafiti yalibaini kuwa mbinu za lugha zinazodhihirika katika nyimbo za mapenzi zilizochunguzwa ni kuchanganya ndimi, takrikiri, Chuku, tasfida, sitiari na tashbihi. Utafiti huu ulipendekeza watunzi wa nyimbo za mapenzi watumie pia mbinu nyingine za lugha kama vile methali ambayo haikujitokeza sana. Watafiti wengine pia wafanye utafiti kuhusu mbinu za lugha kwenye aina nyingine za nyimbo. Utafiti huu utakuwa wa manufaa kwa vyombo vya habari haswa stesheni za redio ili wafahamu mchango wao kwa ujenzi wa lugha ya Kiswahili kwani wao ndio husambaza na kucheza nyimbo hizi za mapenzi. Vilevile utafiti huu utakuwa na mchango katika kuleta ushirikiano mzuri wa kiakademia katika jumuiya ya Afrika mashariki kwa vile ilitafiti nyimbo kutoka Kenya, Uganda na Tanzania